SERENA WILLIAM; TUZO NA MAFANIKIO YAKE HAVIKUTOKEA KAMA AJALI
NI mcheza tenesi wa kimataifa kutoka Marekani, anashika namba moja duniani kwa upande wa wanawake na anatajwa kuwa mcheza tenesi bora wa muda wote.
Alianza kuwa mchezaji wa tenesi bora wa kwanza duniani Julai 8, 2002. Mwaka, 2015, alikuwa ni mwanamichezo wa pili wa kike kulipwa pesa ndefu duniani akikunja dola za Kimarekani milioni 24.6 ambazo ni zaidi ya bilioni 50 za Kitanzania.
Kama haitoshi Julai 18, 2016 alitajwa kuwa mcheza tenesi bora namba moja duniani kwa wiki 179 mfululizo. Lakini pia amefanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mcheza tenesi wa kike pekee kuchukua tuzo 10 za Grand Slam katika miongo miwili tofauti.
Hata hivyo, tuzo yake ya 38, katika tuzo mbalimbali alizowahi kuvuna ilimfanikisha kuwa namba nne katika listi ya wacheza tenesi wa muda wote, lakini namba mbili kwa wacheza tenesi ambao bado wanashiriki kwenye mchezo huo.
Ni nani huyu? Si mwingine bali ni Serena Williams, mdogo wa damu wa mcheza tenesi bora duniani, Venus Williams na mama wa mtoto mmoja aitwaye Alexis Olympia Ohanian Jr.
Serena ana historia ndefu sana katika mchezo wa tenesi, lakini mapambano yake ndiyo yamemuwezesha kupata mafanikio aliyonayo na sifa kote duniani wala haikutokea kama ajali.
Kwa wanawake wengine wa chuma, bila shaka wana mengi ya kujifunza kwa mwanamke huyu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 31. Na katika vitu vya kujifunza, kwanza kabisa ni kujiamini kwamba unaweza, kupigania ndoto, kila siku kujitahidi kuwa bora zaidi ya jana, kuwa na nidhamu na kuwa na njaa ya mafanikio.
Tukianza na imani, Serena anasema wakati akiwa mdogo alikuwa akikaa kwenye benchi katika Uwanja wa Tenesi wa Courts, akimshuhudia baba yake akimfundisha dada yake, Venus mchezo huo. Baada ya kutazama kwa muda, siku moja akamwambia baba yake: “Na mimi ninaweza kucheza kama unavyomfundisha dada?”
“Kuanzia hapo ndipo baba alipoanza kunipa nafasi na kuandika hii historia ambayo leo inawahamasisha watu wengi duniani. Na hicho ndicho kitu kizuri katika historia, fanya kazi zako kwa mapenzi, juhudi na nguvu, hufahamu nani historia yako itamgusa na kubadilisha maisha yake,” amewahi kusema Serena wakati akifanya mahojiano na Kituo cha Habari cha CNN.
Serena na dada yake wamekulia kwenye familia ya kimaskini huko Compton, Califonia, Marekani. Wakati wanaanza kupambania ndoto zao, walikuwa wakilazimika kukatiza kwenye mitaa ya vijana wahuni, wakorofi na wasio na makazi ili kwenda kujifua katika Uwanja wa Tenesi wa Courts.
Walifanya mazoezi kwa nguvu kati ya saa tatu hadu nne wakiwa ni wenye juhudi. Kuna wakati walilazimika kuamka asubuhi saa 12:00 na kufanya mazoezi kabla ya kwenda shule na kuendelea na mazoezi baada ya kutoka shule hadi pale giza lilipoingia.
“Sikuwahi kufikiria kwamba nitakuja kuchukua tuzo 21 za heshima duniani na nyingine mbalimbali zaidi ya 38, kwa maana wakati ninaanza sikuwa nina tuzo yoyote.
“Mazoezi kwa miaka 30, hakikuwa kitu kidogo, lakini ilinilazimu kujituma kila siku kwa sababu nilihitaji kuwa huyu niliye leo. Sehemu nilipoona ndipo nimefikia mwisho, sikuruhusu pawe mwisho, palikuwa ni kikwazo tu pakunipigisha hatua zaidi ya kufikia mafanikio yangu.
“Kwa mtu yeyote duniani, kuwa na njaa ya mafanikio. Jitume leo kuliko jana. Amini unaweza na kwamba kile unachokiamini ipo siku kitafanikiwa. Ukiwa na vyote hivi, mafanikio hayawezi kukukwepa,” ni maneno ambayo amewahi kuyasema Serena alipoulizwa kuhusu mafanikio yake.
Bila shaka mwanamke wa chuma umemsoma Serena. Hebu tazama kuhusu wewe ulipo, hii historia yake inawezaje kufanya kazi katika maisha yako ya kawaida.
Usijali hata kama ikiwa umeanguka bila idadi, unaweza kuamka na kuanzia hapo ulipo na kusonga mbele. Kitu kibaya katika maisha huwa hatuwezi kurudi nyuma na kusahihisha kule tulipokosea au kudondoka, lakini kizuri zaidi tuna uwezo wa kurekebisha kuanzia tulipo na kusonga mbele.Inuka kwa matumaini na imani, sema unaweza. Pambana mpaka kieleweke.
Makala: Boniphace Ngumije