ANGALIA MWANAMKE AMBAYE NI SHABIKI WA KOCHA JOSE MOURHINO,AMFANYIA MATUKIO YA AJABU
Shabiki wa soka, Vivien Bodycote, 59, ameamua moyo wake ufanye kazi mbili kwa wakati mmoja, kwanza ni kusukuma damu, pili ni kuhifadhi upendo wake kwa Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho. Inawezekana hilo likawashangaza wengi lakini ukweli ndiyo huo kuwa Vivien ni shabiki mkubwa wa kocha huyo raia wa Ureno ambaye pia ni baba wa watoto wawili.
Vivien hajaficha hisia zake, bali ameziweka wazi kiasi kwamba hata mumewe, Tony ambaye ana umri wa miaka 76, anafahamu jinsi mkewe anavyomkubali kocha huyo na ndiyo maana wawili hao wametumia zaidi ya pauni 800 (Sh milioni 2.3) kuchora tatuu zenye taswira au zinazohusiana na kocha huyo. Akielezea zaidi, Vivien anasema: “Huwa ni nadra kwangu kwenda mjini kisha nirejee nikiwa sina tatuu ya Jose mwilini mwangu, nina tatuu 20 zinazomhusu yeye.
Siyo kwamba ni mtu muhimu, ni mtu wa kipekee kwangu. “Nitafurahi sana nikikutana naye, nipo tayari hata kumsaliti mume wangu linapokuja suala la Mourinho. Ni mtu mwenye mwonekano wa tofauti, kila mara ninapofunua gazeti na kumuona huwa napata washawasha kwenye magoti. “Bei za tatuu zangu zipo tofauti, kuna ambazo nilichora kwa gharama ndogo ya pauni 60 (Sh 171,850) lakini nyingi ni za pauni 250 (Sh 716,040).
Kwa jumla zimenigharimu kama pauni 800.” Vivien ambaye ni mkazi wa mtaa wa Hinckley Kitongoji cha Leicestershire hajawahi kwenda uwanjani tangu alipofanya hivyo miaka ya 1900, alipoenda akiwa na baba yake ambaye kwa sasa ni marehemu lakini hiyo haijamzuia kuwa shabiki mkubwa wa soka. Shabiki huyo ambaye umri umemtupa mkono ni bibi mwenye wajukuu, alifunga ndoa na mume wake wa sasa miaka 15 iliyopita, ameongeza: “
Hakuna siku ambayo inapita bila mimi kuitazama picha ya Jose mtandaoni, nimeathirika kwa Jose Mourinho. “Nimekuwa nikiulizwa na majirani kuwa kwa nini nisiwe shabiki wa Leicester lakini mimi ambacho ninawajibu ni kuwa nipo kwenye penzi zito na kocha huyo wa soka. “Kama akiamua kuondoka Manchester United kwenda nje ya nchi kufundisha hata mimi pia nitaacha kushabikia soka la Uingereza, nitamfuata huko atakapokwenda.
Mjukuu wangu aliponiambia wakati Jose alipofukuzwa Chelsea, nilifuta sherehe zote za Krisimasi na hakukuwa na mlo wa usiku kipindi hicho, nilitamani kukutana naye na nimweleze hisia zangu jinsi nilivyoumia, nimpoze.” Ajabu ni kuwe, mume wa Vivien ndiye ambaye amekuwa akitoa fedha ili mkewe akajichore tatuu hizo za Mourinho kutimiza furaha yake.
Akizungumzia hali hiyo, Tony anasema: “Anafanya anachopenda huwa sijali kuhusu kumuongezea fedha au kumpa fedha za kujichora tatuu, najua zina gharama kubwa lakini sijui gharama yake halisi. “Sijawahi kupenda mpira na wala siyo shabiki wa mchezo huo lakini miaka michache iliyopita ndipo nilipoanza kufuatilia kidogo japokuwa sikuwahi kwenda uwanjani, lakini yeye (mkewe) anapenda.” Upande wa bibi mwenyewe anasisitiza kwa kusema: “Nimekuwa sifikirii idadi ya tatuu nilizonazo kwa kuwa kila ninapomaliza kuchora moja huwa nafikiria nyingine.
Tony huwa ananipeleka sehemu za kuchorea na kuniacha.” Kuna tatuu ambayo ameiandika Mrs Mourinho akimaanisha yeye ndiye mke wa Mourinho kisha pembeni yake kuna tatuu ya sura ya Mreno huyo. Maisha ya Mourinho Mourinho ni mume wa Matilde ‘Tami’ Faria, uhusiano wao ulianza tangu wakiwa vijana walipokutana Setúbal nchini Ureno. Walifunga ndoa mwaka 1989. Mtoto wao wa kwanza, Matilde alizaliwa mwaka 1996, wa pili, José Mário, Jr.
alizaliwa miaka minne baadaye. Kuhusu imani yake, Mourinho aliwahi kunukuliwa akisema: “Mimi ni Mromani Katoliki, namuamini Mungu, nasali kila siku, kila siku nazungumza na Mungu, huwa siendi kanisani kila siku wala kila wiki, huwa ninaenda ninapojisikia.
Kutokana na imani yake hiyo, Mourinho haruhusiwi kuoa wake wawili, hivyo hata kama Vivien akimfuata na kumueleza nia yake, haitawezekana. Mourinho anazungumza Kireno, Kihispania, Kifaransa, Kicatalan (Barcelona) na Kingereza. CHANZO: CHAMPIONI